KUPUNGUA kwa bei za makampuni mbalimbali kumechangia idadi ya mtaji
wa soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kushuka kwa asilimia nne.
Akizungumza jana kuhusu taarifa ya soko katika mauzo yaliyofanyika
wiki iliyopita, Meneja Miradi na Biashara wa DSE, Patrick Mususa,
alisema idadi ya mtaji wa soko imeshuka kutoka Sh trilioni 21.0 hadi Sh
trilioni 20.2.
“Kiasi hicho kinaonesha kuwa bei za hisa za makampuni zimepungua kwa
asilimia 3.9,” alisema Mususa wakati akitoa taarifa ya DSE kwa mnada
uliofanyika wiki iliyopita.
Aliongeza kuwa idadi ya mtaji wa makampuni ya ndani imeshuka pia kutoka Sh trilioni 9.7 hadi Sh trilioni 9.4.
Katika mnada huo, Benki ya CRDB ilichangia zaidi ya asilimia 75 ya
idadi ya mauzo yote ya wiki iliyopita, ingawa bei ya hisa zake ilishuka
kwa asilimia 1.23.
Alisema idadi ya mauzo ya hisa, imeongezeka wiki iliyopita
yameongezeka kwa asilimia 50 hadi kufikia Sh bilioni 6.7 kutoka bilioni
4.4.
Idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa, imepanda zaidi ya mara nne hadi Sh milioni 12.8 kutoka milioni 3.6.
Alitaja kampuni tatu zinazoongoza kwa idadi ya hisa zilizouzwa kuwa
ni Benki ya CRDB kwa asilimia 98.45, Kampuni ya Bia (TBL) asilimia 0.75
na Kampuni ya Saruji Tanga (TCCL) kwa asilimia 0.34.
“Hii inaonesha kuwa CRDB ilichangia zaidi ya asilimia 75 ya idadi ya
mauzo ya wiki hii ingawa bei yake ilishuka kwa asilimia 1.23,” alisema
Mususa.
Kwa upande wa viashiria, Mususa alisema kiashiria cha sekta ya
viwanda kimeshuka kwa pointi 4.33, kikiwa kimechangiwa na punguzo la bei
ya hisa kwenye kaunti za TCCL kwa asilimia 0.75 na Kampuni ya Saruji ya
Twiga (TPCC) kwa asilimia 0.67.
Alisema kiashiria cha sekta ya huduma za kibenki na za kifedha,
kimeshuka kwa pointi 113.23, kikiwa kimechangiwa na punguzo la bei ya
hisa kwenye kaunta za Benki ya NMB kwa asilimia 6.12 na CRDB kwa
asilimia 1.23.
“Kiashiria cha sekta ya huduma za kibiashara kimeshuka kwa pointi
16.75 kikiwa kimechangiwa na punguzo la bei ya hisa kwenye kaunta ya
Swissport kwa asilimia 0.55,” alisema Mususa.