RAIS John Magufuli amemhakikishia Waziri Mkuu wa Israel kuwa Serikali
ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari
kushirikiana na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Israel
katika nyanja mbalimbali ili kuleta manufaa kwa pande zote.
Rais Magufuli alisema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na
Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Yahel
Vilan, Ikulu jijini Dar es Salaam. “Natambua mahusiano mazuri yaliyopo
kati ya Tanzania na Israel, mahusiano haya ni muhimu sana kwa ustawi wa
nchi zetu mbili, nataka mahusiano haya yaimarishwe zaidi,” alisema Dk
Magufuli.
Aidha, aliahidi kuwa Tanzania itahakikisha inaanzisha ubalozi wake
nchini Israel haraka iwezekanavyo. Kwa upande wake, Balozi wa Israel
nchini, Vilan pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri
iliyofanywa na uongozi wake katika kipindi kifupi cha miezi miwili
tangu aingie madarakani, amemhakikishia kuwa Israel itaendelea
kushirikiana na Tanzania na ipo tayari kuimarisha zaidi mahusiano.