MIRADI mitatu yenye thamani ya Sh milioni 445, imetiwa saini baina ya
Serikali ya Japan kupitia ubalozi wao nchini kwa ajili ya uendeshaji
miradi mitatu katika mikoa ya Arusha, Unguja na Morogoro.
Miradi hiyo ni ujenzi wa shule ya msingi Kingolwira Manispaa ya
Morogoro, ujenzi wa uzio wa shule ya msingi Muyuni iliyopo Wilaya ya
Kusini Unguja na pamoja na kuiwezesha vifaa Hospitali ya Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ya Selian jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini makubalino hayo, Balozi wa
Japan nchini, Masaharu Yoshida alisema wametoa msaada huo ikiwa ni
mwendelezo wake wa kusaidia miradi ya kijamii kama afya, elimu na maji.
Balozi Yoshida alisema mradi wa kwanza ni wa upanuzi wa shule ya
msingi Kingolwira iliyojengwa tangu mwaka 1952, ambayo majengo yake ni
chakavu na hivyo kufanya watoto na walimu kusoma katika mazingira
hatarishi.
“Shule hii ilijengwa miaka 63 iliyopita, majengo yake kwa sasa ni
chakavu na yanahatarisha usalama wa watoto na baadhi ya madarasa yamejaa
watoto zaidi ya 180 na wengi wao wakiwa wamekaa chini na walimu wakiwa
wamekaa chini ya miti,” alisema Balozi Yoshida.
Alisema kiasi cha dola 86,182 sawa takribani Sh milioni 190
zitatumika katika ujenzi wa madarasa matatu, ujenzi wa ofisi za walimu
na vyoo shuleni hapo.
Mradi mwingine ambao utagharamiwa ni ujenzi wa uzio katika shule ya
msingi Muyuni Wilaya ya Kusini Unguja Mjini, ambao utagharimu dola
29,799 ambazo ni sawa na Sh milioni 64.
Balozi Yoshida alisema kukosekana kwa uzio katika shule hiyo,
kunafanya watu kupita na kuathiri watoto wakiwa darasani wakiendelea na
masomo.
Mradi mwingine ambao Serikali ya Japan imetia saini kuwezesha ni ule
wa kuisaidia Hospitali ya Selian jijini Arusha, vifaa tiba ambao
utagharimu dola 88,319 sawa na Sh milioni 192.
Wakizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo, wawakilishi
kutoka taasisi hizo waliahidi ubalozi wa Japan, kuitumia misaada
waliyopata kama ilivyo kusudiwa.
Mwakilishi wa Hospitali ya Selian, Samuel ole Saigura alisema msaada
huo utatumika kununulia vifaa tiba na kuboresha huduma katika idara ya
wagonjwa mahututi (ICU) hospitalini hapo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Theresia Mahongo alisema kuwa
msaada huo utawanufaisha walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi
Kingolwira na utaleta manufaa kwa wakazi wote wa Mkoa wa Morogoro na
taifa kwa ujumla.