POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia wananchi kadhaa,
wakituhumiwa kufanya fujo na kufunga barabara ya Kawawa kwa muda na
kuchoma matairi.
Kukamatwa kwa watu hao, wanaosadikiwa ni wa Bonde la Mkwajuni jijini
Dar es Salaam, kunatokana na kile kilichodaiwa ni kufunga barabara baada
ya maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
kuweka alama ya X katika vibanda walivyojenga watu hao kwa ajili ya
makazi.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Simoni Sirro alisema wakazi hao
watahojiwa kueleza sababu za kufunga barabara hizo na kusababisha
kukosekana kwa mawasiliano.
Vurugu hizo zilizotokea jana saa 6 mchana, inadaiwa zilisababishwa na
baadhi ya vijana wanaoishi katika maeneo hayo, ambao walichoma matairi
pande zote za barabara na kusababisha foleni na usumbufu kwa watumiaji.
Polisi na gari la zimamoto lilifika eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha
usalama wa watumiaji wa barabara hiyo na wananchi wengine.
Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventura Baya
alisema walichofanya wananchi hao, si sahihi kwa kuwa walishaelezwa
kwamba vibanda hivyo vingeondolewa katika eneo hilo.
Akielezea kilichojiri, Baya alisema jana asubuhi alikwenda eneo hilo
kwa ajili ya kukagua kazi iliyofanywa na wafanyakazi wake na alipokuwa
anaondoka, aliona vijana wanarusha mawe na kuchukua mbao na matairi na
kuchoma moto katikati ya barabara.